The Jim Harries Mission Page
Home

News

Rundbrief

Jim's Work

Articles

Links

Contact Us

Journal

Discussions

Pasipo Kujua Mila yake Huwezi Kujadiliana na Mtu Barabara

(The (Im)possibility Of Inter-Cultural Dialogue)

Mata ya Maarifa itakayotolewa kwenye chuo cha kimataifa cha theologia kilicho Kima, Kisumu, Kenya, tarehe 19.09.07 Mnenaji: Dkt. Jim Harries

Maarifa Lecture presented to the students and staff of Kima International School of Theology, Kisumu, Kenya on 19th September 2007. Presenter: Dr. Jim Harries

(Yanalingana na tolea ya Kiingereza inayoitwa: Intercultural Dialogue - an overrated means of acquiring understanding examined in the context of Christian Mission to Africa.

Utangulizi

Kujadiliana, inafahamika na wengi, kunaleta ufahamu na usuluhisho wa mambo mbali mbali. Inaaminiwa kuwa hivyo hata kati ya watu wanaotoka kwenye mila tofauti. Ninapinga. Nasema mijadala kati ya watu wenye mila mbali mbali, wasipofahamiana kimila, ni upotevu. Mara nyingi ni kuachiana njia, na sio kufahamishana zaidi. Kwa hivyo mmisionari, ili awafikie watu wenye mila kigeni, lazima ajihusishe na hiyo mila yao, pamoja na lugha yao.

Watu wawili kujadiliana juu ya kitabu fulani kinaweza kuwafurahisha na kuwanufaisha wote wawili; ikiwa wote wawili wamekisoma kitabu kimoja. Lakini ikiwa vitabu walivyosoma vilikuwa tofauti hawataelewana, wasipo tangulia kwanza kufundishana au kurekebisha lile kosa. Wawili wakiongea juu ya mchezo, lakini mmoja juu ya mpira na mwingine juu ya voliboli, hawataelewana. Mmoja akiongea juu ya ufugaji wa kuku na mwingine uchungaji wa ng'ombe, hawataelewana.

Tena watu wawili wakiongea lakini kila mmoja akitumia lugha ambayo mwenzake hajui, kwa mfano lugha mmoja ni Kiluo na nyingine Kiluiya, hawataweza kuelewana. Mluiya akiongea na Mkikuyu ni afadhai sababu hizi lugha zinafanana. Bora kabisa waongee lahaja moja ya lugha moja.

Uelewano unahitaji vitu viwili - lugha iwe moja, na jambo litakalohusika katika mjadala liwe ni moja. Lugha moja na jambo (au mila) tofauti, au mila moja na lugha ikiwa tofauti, na mijadala italeta ufanisi kidogo.

Tufahamu pia; kuelezwa juu ya mchezo au kuambiwa juu ya kitabu fulani, ni tofauti na kuucheza ule mchezo au kukisoma kile kitabu chenyewe. Ni vigumu kuamini mtu anaweza kuwa mchungaji mwema wa ng'ombe kabla hajawachunga hata siku moja. Kwa uhakika - kukifahamu kitu kigeni kinatokea kwa kukifanya au kukiona na macho, na sio tu kwa kuambiwa kuhusu kitu hicho.

Tunaweza kusema mijadala inayonufaisha kawaida inatokea kati ya watu ambao ufahamu wao unalingana. Nataka tuchunguze kwa undani kidogo - hali inakuwaje?

Lugha iwe sawa/moja

Pasipo ukalimani, mjadala unatakiwa uwe katika lugha moja. (Tutaona - hata ukalimani ukiwepo, bado lugha moja itahitajika.) Uchaguzi wa lugha unaonekana kuwa muhimu.

Tutalinganisha Waluyia na Waluo tukiangalia tu maneno mawili- dala / ingo (boma) na kuon / obusuma (ugali). Tunajua jinsi Waluo wanapanga boma zao tofauti na ujenzi 'ovyo ovyo' wa Waluyia.1 Tuseme (kwa mfano wetu) kuon inatengenezwa kwa mhogo, lakini obusuma kwa mahindi. Tukija sasa kwa uchaguzi wa lugha, tunatakiwa tujiulize maswali mawili: 1/ Lugha gani? 2/ Mila gani? Je, Mluo akiwa kwa Waluyia akiomba obusuma atafahamika, je anauhitaji ugali wa mhogo au wa mahindi? Akisharudi nyumbani akisema anataka kutoa ingo swali litakuwa - atajenga kimpango, au atatengeneza boma ovyo ovyo? Kumbe kitu muhimu sio lugha itakayotumiwa, lakini makubaliano juu ya mila itakayokuwa inafahamika inapotumiwa katika hiyo lugha!

Matatizo bado yanawezakuwepo hata watu ambao wanatumia lugha mbili wakikubaliana kwa mila moja (na wakiwa wanafahamu hiyo mila moja), kwa sababu jinsi vitu vinavyotajwa inategemeana na lugha. Mluo anayezuia kusema apenji (Kiluo: mimi-uliza-wewe) atakutana na kazi ngumu kupata maneno yenye maana moja kwa lugha zingine. Pengine Mluo akisema 'hebu' inafahamika kwamba anajaribu kusema apenji? (Ni vigumu kupata mifano ya aina hiyo kati ya Kiingereza na Kiswahili sababu Kiingereza cha Kenya kinafuata sana Kiswahili.)

Lakini, sababu ni mila inayodhaniwa kuwa muhimu hata kushinda lugha inayotumiwa, inakuwaje ikiwa wanaoongea wasipofahamiana kimila? Kusema ukweli, hata wakiwa wanajua 'lugha moja', bado hawataweza kufahamiana barabara. Mahali maelewano yanakosekana inaweza kuwa jambo la muhimu. Ugali unaotengenezwa na mhogo ikidhaniwa ni mahindi inaweza kuwa ni sumu. Mluo akitengeneza boma ya ingo badala ya dala itajulikana watu wake wataweza kufa kwa wingi.

Tunaweza kusema nafasi ya kushirikiana kilugha kwa watu wanaotofautiana kimila - ni nadra sana!

Wadukizi na Wasikilizaji Wasioonekana

Dialogue, kulingana na asili yake ya Kigriki, ni maongezi kati ya watu wawili. Kweli maongezi kati ya watu wawili yanaweza kuwa tamu. Lakini je, inawezekana?

Mkubwa wa shamba anaweza kuwa na wafanyakazi wake. Tuseme anamwita mmoja na kumwambia "unahitaji ulale papo hapo kazini" sababu siku hiyo ng'ombe fulani atahitaji msaada wake akizaa. Mfanya kazi atastuka na kujitetea. Ikionekana mkubwa wake hamsikilizi, ataweza sema: "nilimwahidi jirani wangu ili nimsaidie kutengeneza baisikeli ili kesho yake ampeleke mkewe anayeugua hospitalini". Sasa, mjadala uliyokuwa kati ya watu wawili umehusisha watu watatu, au wanne (jirani na mkewe)! Ili mkubwa aweze kumshawishi mfanya kazi abaki hapo sasa haimhitaji tu kumfahamu mfanyakazi mwenyewe, bali pia wale watu na hali zao.

Hawa wawili wakishaletwa kwa mjadala, sasa itakuwaje kwa wengine? Pengine mke wa mfanyakazi hana ufunguo wa chumba chao cha sitor yao. Pengine mtoto wake alitarajia kupewa pesa ili alipe mtihani, na hiyo ilikuwa siku ya mwisho. Pengine mama mzazi alimwonya kutolala kazini sababu mkewe ni mwenye wivu sana. Lakini pengine baba yake ambaye ni marehemu alimwambia kazi ni maisha ya mtu na lazima iwe kitu cha kwanza kufikiriwa. Hata wafu wanaweza kuhusika katika mjadala ule! Akiwa anaongea na mkubwa wake shetani mwingine (mzimu) anaweza kuja kumwonya asilale hapo au atamwua! Kumbe, mjadala kati ya watu wawili tu, haupo!

Kawaida, nikimfahamu mtu ambaye ninajadiliana naye, na watu wake, na hali na mila yao, sitastushwa sana na hao watu wengine. Lakini nisipowafahamu itakuwa rahisi kwangu kushindwa kufikisha lengo langu (mfanyakazi awe karibu ili amsaidia ng'ombe akizaa) nikiongea na huyu mtu.

Tunaambiwa na watalamu; pesa ambayo inatumwa na wafadhii inatakikana kutumiwa kulingana na matakwa yao. Lakini tunagundua mara nyingi haifanyi hivyo. Kwa nini? Kwa sababu mgeni (Mzungu) anayetuambia kufanya hivyo ni wa hawa, lakini hawa siyo wetu. Tunaweza kusema, Mzungu anapojadiliana 'wako naye'. Lakini mwenyeji atakayechukua uongozi kutoka kwake hatawaona hawa watu, kwa hivyo hatawajali kiasi cha huyu ambaye ni mtu 'wao'.

Inakuwaje mtu akiwa na uhusiano na mizimu? Wafu huongee naye, wanamsikiliza kwa kila jambo, na wanao uwezo wa kumwumiza! Nadhani itakuwa kama mtu akiwa na wachumba wawili ambao hawajatambuliana, akikutana nao wote wawili sehemu moja. Wasipogundua siri ambayo mzee anajaribu kuficha, watashindwa kuvifahamu vitendo vyake vya kuhepa, kunyamaza, na kuwa na hofu anapojadiliana nao! Au tuseme mnamba wa matatu anamwelezea dereva wake kwa furaha jinsi wanakwepa polisi, na huku dereva anaona polisi akasimama nyuma yake, lakini mnamba hajatambua! Hata mwanafunzi wa KIST akiongea juu ya Mkuu wa chuo, bila kujua mwenyewe kwamba amekuja na amesimama mlangoni mwa chumba. Mdukizi mwingine ambaye uwepo wake unakubaliwa na kila Mkristo ni Mwenyezi Mungu Yehovah. Uwepo wake ni lazima utaathiri hali za mijadala.2

Kujitakia Hali, au Siasa

Siasa (kushindana kwa uwezo ndani ya jamaa au umma fulani) mara nyingi haipo kwenye maneno, lakini kwa mazingira au muktadha. Bush hajasema anavamia Iraq sababu ya mafuta mengi yaliyomo, lakini bado watu wengi wanaweza kufikiri ni hivyo. Muuzaji halazimishwi kumwambia mteja wake "ninataka nipate mali nyingi iwezekanavyo kwako", lakini mnunuaji awe macho akienda kununua kikapu sokoni Luanda akiambiwa alipe elfu tano! Mvulana akimpa msichana mandazi hakuna haja ya kumwambia "ninakuchumbia". Kwa kawaida mazingira yanatosha kumfahamisha maana ya kitendo.

Uhusiano kati ya makanisa hapa Afrika na ya Ulaya siku hizi unakuwaje? Mzungu akija Kenya akitafuta wachungaji ili ahusiane nao, je, mtamkaribisha kuhubiri kanisani kwako? Ukikutana naye utamwambia kitu utacholenga sana sana ni pesa yake, au utamwambia wewe unahaja na roho za watu sio mali ya dunia? Utamfinya mpaka pesa itoke (wewe usipofanya hivyo mwingine atachukua nafasi hii), na bora ajue ni wewetu unayempenda Yesu kwa ukweli (viongozi wa makanisa mengine wamepotea) inchini. Biblia haielezi jinsi Yesu alivyowafanyia wageni kutoka Ulaya walipofika kwake, lakini kwa sisi ni kawaida, ila hatusemi!

Mtu anaweza kusema kitu bila kugundua. Kuongea sana juu ya chakula mezani magharibi ya Kenya nimegundua kwamba inaweza leta tashwishwi au kukwaza. Lakini kufanya hivyo ni kawaida kwa Waamerika. Wanafunzi wa KIST nimesikia wakijitetea wakimwambia mgeni kutoka Amerika mama yao anaugua sana na hana pesa ya kulipa kwa ajili ya matibabu hospitali (ili amwombee) walishitakiwa baadaye kwa ajili ya kuomba omba wageni. Mtu akiniambia "mkutano wetu utakuwa 'saa tatu kamili'" siku hizi mimi nachanganyikiwa tu (sijui utakuwa saa ngapi)! Nikipokea barua pepe inayonitaarifu nitapewa Ksh6,000,000, ninahaki nikiwa na shaka sababu kawaida aliyenitumia email anahaja na pesa zangu - lakini hasemi hivyo!

Sababu ubishi mwingi wa siasa haupo kwenye maneno lakini kwa kufahamu muktadha, hayo mambo hayatafsiriwa hata lugha ikitafsiriwa.

Hali ya Mawazo

Kila mtu anakuwa na njia yake ya kipekee kuwaza. Kila mwanaume anajua - yeye ndiye sawa au hata bora. Watu fulani wanao mbinu au mawazo ambayo ni tofauti na watu wengine. Mbinu za kuwaza za watu wanaotoka Ulaya ni tofauti na mbinu za wenyeji wa Kenya. Kwa hivyo mawazo yanayo simamia (kuwa msingi wa) maneno yanakuwa tofauti.

Mtu kutoka Ulaya akisema "mnahitaji maendeleo kanisani" anamaanisha "fanyeni vile sisi tunavyofanya na tulivyofanya, na sisi tutatoa msaada". Lakini Mkenya ambaye ameishi Kenya (Tanzania, Uganda n.k) hawezi jua jinsi mambo yanavyokuwa kule Ulaya! Yeye anajua maendeleo yanakuja wageni wakija kwa wingi, na yanatokana na baraka. Lakini hatakubali kutofahamu mambo ya Ulaya akihofia ataonekana mjinga, au ule msaada unaweza kutolewa.

Hali kadhalika tukiangalia neno la 'dawa'. Dawa inatumiwa na mtu akiwa amelogwa, akiwa na chira (chisila), akisumbuliwa na mapepo au akiwa na bahati mbaya, ili izuie hizo nguvu za uharibifu. 'Dawa' ya mzungu inatumiwa kuwapiga vijimelea vidogo sana mwilini ambao hawaonekani hata kwa macho. Ni vitu tofauti sana, lakini jina linalotumiwa ni moja. Kwa hivyo Mtanzania anadhania hata dawa ya mzungu inapiga wachawi, na Mwulaya anadhania dawa ya Uganda inawalenga vijimelea hawa kama dawa yake!

Vitu vingine havifikiriwa hata, na haviongelewi. Pale Ulaya hakuna mtu ananiuliza jina la Baba na Babu yangu. Nikiwa Siaya watu huuliziana saa yote! Kuuliza juu ya watoto wa mtu kinaga ubaga ukiwa Ulaya kinaonyesha unawajali, lakini kuthubutu kufanya hivyo ukiwa Siaya na utadhaniwa kuwa mchawi.

Hitimisho

Mijadala kati ya watu wasiofahamiana kimila inaleta kubuni na kuunda hali fulani mawazoni juu ya mtu ambaye hayapo duniani. Kuitumia hali iliyobuniwa ili utoe shauri kwa lugha yako kunawasaidia watu hawa wa mila tofauti na wako, inawezakuwa upuuzi.

Ugunduzi huo unatubidi tufikirie tena kazi ya kanisa kwa bara la Afrika. Kanisa linawezaje kuongozwa na lugha ambayo mizizi yake iko mbali? Hali hii inaleta mchanganyiko. Ili mijadala iwe barabara lazima wahusika wawe na hali ya mila inayofanana. Inter-cultural dialogue ni ubunuzi na upotevu. Haiwezekani. Kazi ya umisionari ili ifanywe kwa ukweli na udhabiti sio kuyarusha maneno ili yavuke mipaka ya mila, lakini ni ya mtu mwenyewe kuvuka mpaka ili aweze kupeleka injili kwa walengwa kupitia lugha yao na kulingana na mila yao.

Hatua moja inayohitajika ili kuwezesha hali hii, ni lugha ya Afrika kutumiwa kwa elimu ya theologia Kiafrika. Hii peke yake inaweza kuliokoa kanisa Afrika kwa mikono ya wale ambao, hata ikiwa wanadhania wanafanya kazi njema, wanaathiri ukuaji wake.